Ticker

6/recent/ticker-posts

REA YAAHIDI KUENDELEA KUSIMAMIA FEDHA ZA MIRADI KULETA MATOKEO YALIYOKUSUDIWA



Na Mwandishi Wetu - Mafia, Pwani


Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha fedha zinazotolewa na Wabia wa Maendeleo zinatumika kutekeleza miradi ya nishati yenye tija kwa wananchi, sambamba na kufanikisha malengo ya Serikali katika kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa wananchi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Said, wakati wa ziara ya Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati walipotembelea kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA katika Visiwa vya Chole, Juani na Jibondo mkoani Pwani.

Mhandisi Said amesema REA imekuwa na utaratibu wa kufanya vikao hivyo mara mbili kwa mwaka, kikiwemo kikao cha kupanga utekelezaji wa miradi kwa mwaka wa fedha husika na kingine cha kukagua maendeleo ya miradi iliyokubaliwa kwa pamoja, hatua inayowapa wadau wa maendeleo fursa ya kuona matumizi ya fedha zao na matokeo yaliyopatikana kwa wananchi.

Amesema ziara hiyo imewawezesha wadau kujionea utekelezaji wa mradi mkubwa na wa kipekee wa kusambaza umeme visiwani kwa kutumia nyaya zinazolazwa chini ya bahari, maarufu kama ‘Submarine Cables’, ambao unatarajiwa kuhudumia takribani vitongoji 11 katika visiwa hivyo, ikiwemo vitongoji sita vya Jibondo.

Ameongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya umeme, huku akieleza kuwa wadau wa maendeleo wamefurahishwa na maendeleo ya mradi pamoja na ushuhuda wa wananchi kuhusu manufaa ya nishati hiyo katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila, amewataka wananchi wanaonufaika na miradi ya umeme kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu ya nishati, zikiwemo mashine umba (transfoma) na nguzo, ili kuepusha vitendo vya wizi na uharibifu vinavyoweza kusababisha kukatika kwa huduma kwa muda mrefu.

Rwebangila amesema miradi hiyo ni mali ya wananchi, hivyo ni wajibu wa jamii kushirikiana na viongozi wa serikali za vijiji katika kuhakikisha miundombinu inalindwa ili Serikali iweze kuendelea kuwafikia wananchi wengine ambao bado hawajapata huduma ya umeme.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, amesema REA imetoa shilingi bilioni 6.8 kwa ajili ya kufanikisha mradi wa kupeleka umeme katika maeneo hayo ya visiwani.

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutumia fursa ya kupatikana kwa umeme kujiandaa kuunganisha huduma hiyo katika nyumba na shughuli zao za uzalishaji, ili kunufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.

Akizungumza kwa niaba ya Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati, Mtaalamu Mwandamizi wa nishati kutoka Benki ya Dunia, Dkt. Rhonda Jordan, amesema wadau wa maendeleo wamefurahishwa na namna wananchi wa Jibondo walivyojiandaa kupokea huduma ya umeme, akieleza kuwa upatikanaji wa nishati hiyo utafungua fursa za kuboresha huduma za afya, kuongeza shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi wa eneo hilo.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo, mkazi wa kisiwa cha Jibondo, Faki Hatibu, amesema upatikanaji wa umeme utachochea kuanzishwa kwa viwanda vidogo vya kuchakata mwani na kuongeza thamani ya mazao ya bahari, ambayo kwa sasa yanachakatwa kwa kutumia teknolojia za kienyeji.

Aidha, mkazi mwingine wa Jibondo, Rehema Ngoma, ambaye ni fundi cherehani, amesema upatikanaji wa umeme utarahisisha shughuli zake za ushonaji kwa kutumia mashine za kisasa zinazotumia umeme.

Amesema umeme utasaidia kuongeza ufanisi wa kazi, kupunguza gharama za usafiri na kuongeza kipato cha wanawake wanaojishughulisha na shughuli za ujasiriamali katika kisiwa hicho.








Post a Comment

0 Comments